Thursday, April 18, 2013

HIVI NDIVYO MAMBO YALIVYOKUA JANA BUNGENI DODOMA


Dodoma.Wabunge watano wa Chadema jana walitimuliwa bungeni na kuamriwa kukaa nje ya Bunge kwa siku tano kutokana na vurugu zilizotokea jana usiku.
Wabunge hao ni Lissu, Hezekiah Wenje (Nyamagana), Highness Kiwia (Ilemela), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini) Godbless Lema (Arusha Mjini) na Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini).
Chanzo za kufukuzwa kwao ni kuwazuia askari wa Bunge kumtoa nje Lissu ambaye alikuwa ameamriwa kutoka nje na Naibu Spika, Job Ndugai baada ya kuingilia hotuba ya Mbunge wa Iramba Mashariki, Mwigulu Nchemba.
Kutokana na tafrani hiyo, Nchemba hakuweza kuhitimisha hotuba yake hivyo Ndugai alilazimika kukatisha mkutano wa Bunge.Hata hivyo wakati akiahirisha mkutano huo, tayari wabunge hao walikuwa wameshatolewa nje baada ya askari kuongezwa.
Mapema Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba alitoa tusi zito la nguoni wakati wa hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, licha ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kupiga mkwara wa kuwashughulikia wabunge watakaorusha matusi.
Mbali na tukio hilo Lema naye alichafua hali ya hewa baada ya kuwatuhumu viongozi wa CCM akiwamo Rais Jakaya Kikwete kwa udini, madai ambayo Bunge limempa siku saba kuyathibitisha.
Lema aliituhumu CCM na Serikali yake chini ya Rais Kikwete kwa kushindwa kutatua mgogoro wa kidini na badala yake kuwa kama analikwepa tatizo. Alionya kuwa Taifa linapasuka kwa migogoro kutokana na viongozi wa Serikali kushindwa kulishughulikia.
Kauli iliwanyanyua vitini Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge na Uratibu na Sera), William Lukuvi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.
Lukuvi na Jaji Werema walisimama wakidai kuwa Lema alikuwa amemdhihaki Rais Kikwete kwa kauli zake za kumhusisha na masuala ya udini.

No comments:

Post a Comment